Jitihada za kuongeza uzalishaji zinakuwa na mafanikio hafifu kutokana na kutotumia teknolojia sahihi zinazoendana na mahitaji na wakati; Mathalani, matumizi ya zana za kulimia ama zikiwa za mkono au zinazokokotwa na wanyamakazi au matrekta, zimekuwa zikisababisha mmomonyoko wa udongo hasa katika maeneo yasiyo tambarare na kusababisha upotevu mkubwa wa rutuba na kujengeka kwa jasi (hard pan).
Kwenye maeneo yenye mvua chache njia hizo za kilimo cha kukatua ardhi hazitunzi unyevu na kusababisha uzalishaji kuwa wa chini hasa pale panapokuwa na vipindi virefu vya ukame (dry spells) kama ilivyotokea msimu huu wa kilimo katika baadhi ya maeneo nchini ikiwemo Mkoa wa Dodoma.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameyasema hayo leo kwenye ufunguzi wa warsha ya siku tatu ya kujadili kwa pamoja namna bora ya kuendeleza Kilimo Hifadhi nchini iliyofanyika katika ukumbi wa St. Gasper uliopo eneo la Kisasa, Jijini Dodoma.
Hasunga anasema kuwa kwa sababu hiyo basi, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni muhimu kubadilisha mifumo inayotumiwa katika kuandaa mashamba ili kupata matokeo mazuri.
Amewashukuru Washirika wa Maendeleo (Development Partners) pamoja na Wadau wote wa Kilimo Hifadhi waliowezesha kufanikisha warsha hiyo muhimu wakiwemo African Conservation Tillage Network (ACTN), Canadian Food GrainBank (CFGB), Diocese of Central Tanganyika (DCT), na Conservation Farming Unit (CFU) –Tanzania.
Alisema juhudi hizo wanazofanya za kuendeleza Kilimo Hifadhi kwa kushirikiana na Serikali kwa maendeleo ya wakulima na Taifa kwa ujumla, ni sehemu ya mwelekeo wa kufikia Uchumi wa Viwanda kwa kukuza uzalishaji wenye tija.
Aliongeza kuwa jitihada hizo zinaendana na Sera ya Kilimo ya mwaka 2013 na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme – ASDP II) ambazo zinahimiza usimamizi endelevu wa matumizi bora ya maji na ardhi, kuongeza tija na faida katika uzalishaji, biashara na kuongeza thamani ya mazao na kuiwezesha Sekta katika uratibu, ufuatiliaji na tathmini.
